- Ukawa waomba Bunge liahirishwe
KIKAO kati ya
Rais Jakaya Kikwete na Wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)
kilichofanyika mjini hapa kujadili mwelekeo wa Bunge Maalumu la Katiba,
kimejaa siri nzito.
Taarifa
zilizopatikana jana baada ya kikao hicho kilichohusisha wajumbe wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), zinasema wakati wa mjadala na Rais Kikwete, wajumbe
wa Ukawa walieleza umuhimu wa Bunge Maalumu la Katiba kuahirishwa kwa kuwa
taratibu za kuliendesha zimekiukwa.
Baada ya
wajumbe hao kueleza kwa nyakati tofauti juu ya suala hilo, Rais Kikwete alisema
hawezi kutoa uamuzi wa moja kwa moja kwa kuwa suala hilo linahitaji tafakari ya
kina.
“Mjadala ulikuwa mzito kwa sababu baadhi ya wajumbe hasa hasa wanaounda Ukawa walieleza umuhimu wa Bunge Maalumu la Katiba kuahirishwa.
“Baada ya kuelezwa hoja hizo, Rais akasema amewasikia na akasema ngoja akatafakari hoja zao na wao waendelee kutafakari juu ya mapendekezo yao,” kilisema chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina.
Wakati hayo
yakiendelea, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, aliwaambia waandishi wa habari,
kwamba baada ya mjadala mzito walikubaliana kukutana tena na Rais Kikwete
Septemba 8 mwaka huu.
“Ndugu waandishi wa habari, leo (jana) wenyeviti na makatibu wa vyama vya siasa vinavyounda TCD tulikutana na rais kujadili ajenda mbili. Ajenda ya kwanza ilihusu mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba na ajenda ya pili ilihusu mambo ya kuimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Rais amekubali kuangalia mambo tuliyomweleza na akatuomba na sisi wajumbe wa TCD tukayatafakari huku ya yeye akiendelea kuyatafakari ili tukutane Septemba 8 mwaka huu.
“Kwa kuwa jambo hili ni muhimu, tumeunda kamati ndogo itakayoangalia mambo yaliyozungumzwa na kuyatolea ufafanuzi kisha kamati hiyo itawasilisha ripoti yake Septemba 8 tutakapokutana,” alisema Cheyo.
Aliwataja
wajumbe wa kamati hiyo ndogo kuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahimu Lipumba, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wibrod Slaa, Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Kabla ya
Rais Kikwete kukutana na wajumbe wa TCD, wajumbe hao walianza kukutana wenyewe
katika Hoteli ya Dodoma na kujadiliana mambo ya kuzungumza pindi watakapokutana
na Rais Kikwete.
Baada ya
kutoka hapo, walielekea Ikulu ndogo iliyoko Kilimani mjini hapa. Hata hivyo,
kabla Rais Kikwete hajakutana na TCD, inasemekana alikuwa na mazungumzo na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira pamoja na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Wakati huo huo, wajumbe hao walipomaliza kikao
chao na Rais Kikwete, walikutana katika Hoteli ya St Gasper ambako walikuwa na
mazungumzo ya zaidi ya masaa mawili.
Taarifa
zilizopatikana katika kikao hicho zinasema Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania
Bara, Phillip Mangula, nusura achafue hali ya hewa baada ya kuwataka Ukawa
warudi bungeni wakati mazungumzo yakiendelea.
Kwa mujibu
wa taarifa hizo, kauli hiyo ilionekana kuwakera baadhi ya wajumbe wa Ukawa wakiwamo Profesa Lipumba na Naibu
Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya ambao walilazimika kumpinga wazi wazi.
Wakati wa
mijadala ya vikao hivyo, CCM waliwakilishwa na Kinana na Mangula. Chadema
waliwakilishwa na Dk. Slaa pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, alikuwapo Mbatia na Katibu mkuu wake, Mosena
Nyambabe wakati CUF waliwakilishwa Profesa Lipumba pamoja na Sakaya.
Kwa upande
wa UDP alikuwapo Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na mdogo wake Isack Cheyo. TLP
alikuwapo Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema na Fahmi Dovutwa
aliviwakilisha vyama visivyokuwa na wabunge bungeni.
0 maoni:
Post a Comment