MWENYEKITI
wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewashukia wanasiasa
wanaomkejeli kwa kudai kuwa hafai kuwa rais na amesisitiza kwamba wenye
maamuzi juu ya suala hilo ni wananchi na si vinginevyo.
Sitta
alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma wakati akitoa taarifa juu
ya utaratibu wa kupokea mawasilisho ya kazi zilizofanywa na Kamati za
Bunge Maalum la Katiba.
Alisema wapo watu wanaomkejeli na kusema kuwa shughuli ya kuongoza Bunge hilo zimemshinda, hivyo hafai kuwa rais.
Alisema yeye hajaomba urais bali anafanya kazi yake kama Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba na si vinginevyo.
“Nafanya
kazi hii kama Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba; haya mengine ya
rafiki yangu Juma Haji Duni (Makamu Mwenyekiti wa CUF) eti anajaribu
kunipima kwa hoja zilizo duni kabisa,lakini mimi nasema wanaochagua rais
ni wananchi,” alisema Sitta na kuongeza;
“Inawezekana
mwakani wananchi wa Tanzania wakatamani mtu mzima aliyetulia
asiyeogopa wapuuzi,wakatamani mtu makini, mwadilifu basi kama itakuwa
hivyo, wajue tupo na sisi wengine wa kuweza kufikiriwa kwa mambo kama
hayo,” alisema Sitta.
Aliwashukia
watu wanaokejeli Bunge hilo kwa madai kuwa uwepo wa wajumbe wa Bunge
hilo ni kinyume na utaratibu na kusema kuwa wananchi mbalimbali
wamebaini kasoro zilizopo katika rasimu kama wajumbe wa Bunge hilo
walivyoyaona katika kamati zao wakati wakijadili rasimu hiyo.
Alisema
kasoro zilizojitokeza katika rasimu hiyo si jambo la ajabu, wala
kupuuza kazi iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani ilifanya
kazi yake vizuri.
“Tukumbuke
Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na mabaraza zaidi ya
700,walichokileta ni tafsiri yao kuhusu maoni hayo, mnielewe vizuri hapo
na wao walikaa tume wakachambua mengine waliyakataa mengine wakayaacha
mengine wakarekebisha,” alisema na kuongeza;
“Ingekuwa
ni kuleta yote maoni ya wananchi ingekuwa ni book (kitabu) ambalo
hatuwezi hata kulibeba lakini Tume ilifanya kazi yake, lakini kama
ilivyo kazi yoyote ya binadamu ina kasoro za hapa na pale,chombo cha juu
cha Tume ni Bunge hili… lina wajibu wake lenyewe halitarajiwi kutoa
rasimu bali litatoa katiba inayopendekezwa ndio maana katika kipindi
hiki tumeendelea na makundi mbalimbali na ninyi wenyewe mmeona yamekuwa
msaada mkubwa yametoa maoni na mengine yamekubalika ili kuboresha
katiba.”
Aliongeza
kuwa lengo na madhumuni ya wajumbe wa Bunge hilo ni pamoja na katiba
watakayoitunga iwe katiba ambayo itawezesha sheria zitakazokuwa rafiki
kwa Watanzania wote hususan wanyonge,wakulima wa kawaida na
wafanyabiashara wadogo.
Hata
hivyo, aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kutofadhaika na maneno ya
kejeli wanayotupiwa hasa kuhusu posho na mambo mengine kwani yeye kama
mwenyekiti wa Bunge hilo yupo imara.
“Mimi
mwenyekiti wenu nipo imara na kwa hulka yangu mimi hizi kejeli, matusi
ni kama vile maji katika mgongo wa bata haloani kwa hiyo waendelee tu
pengine tunaanza kuwabaini,” alisema na kusisitiza;
“Kuna
rafiki yangu mmoja anaitwa Kubenea (Said),jamani karne za nyuma ya
15,16,17 wafalme wa kule Ulaya walikuwa na watu… wafalme wa Ulaya
waliajiri wachekeshaji kwa malengo mawili moja ni kumsikia mfalme kwa
kila kitu, nyingine ni kuwasema wote ambao mfalme ni wabaya wake kwa
hiyo kuna watu wa namna hii tunaanza kuwaona sasa kama Kubenea ni
mchekeshaji wa mfalme… yeye kuna mfadhili na wafadhili nyuma yake
wanamsogeza mbele kwa sababu wanaona vipaji vyake vya kukubali kufanya
kazi kama hizo; kwa hiyo tuwaone nao kuna njia nyingi za kupata riziki
tuwasemehe tu waendelee na shughuli zao,” alisema.
Awali,
alitoa utaratibu wa shughuli za bunge hilo hasa jinsi ya kuwasilisha
taarifa za kamati 12. Alisema baada ya mwenyekiti kuwasilisha taarifa ya
kamati yake kwa sura zote kamati ya uongozi imepanga kila siku katika
ya siku tano za kupokea taarifa wenyeviti wote watapitia sura
zilizoteuliwa ambapo kwa jana walipitia sura namba 2,3,4 na 5.
Sitta
alisema sababu ya kufanya hivyo ni pamoja na kuwa na uangalifu wa sura
chache chache kuliko kamati moja kumaliza sura zote kwani kwa kufanya
hivyo itakuwa na mambo mengi.
Aliongeza kuwa maoni ya wengi yatasomwa kwa dakika 20 huku ya wachache yakisomwa kwa dakika 10.
0 maoni:
Post a Comment