SANTULI YA MIZENGO PINDA HAINA KIBWAGIZO


NA GORDON KALULUNGA.
(Maandishi hayo yametengenezwa, picha hii inasambazwa kwenye whats aap).
ZAMANI za pontio Pilato, mama jusi wa mashariki, walipopita katika himaya ya Mfalme Herode, mfalme akaanza kuhangaika na kujiuliza kuwa kwanini mwana wa Adamu kazaliwa katika nchi ya kiyahudi.
Mwaka 2015 kutafanyika uchaguzi mkuu nchini Tanzania. Tayari baadhi ya mama jusi wameanza kutangaza nia zao za kutaka kuwa viongozi wa taasisi ya Ikulu, majimbo na kata.
Waliopo madarakani baadhi wanajiuliza kwanini wenzao nao wanataka nafasi walizonazo, huku wakisahau kuwa kabla yao walikuwepo wengine.
Mwaka huo ni mwaka ambao waandishi wa habari na baadhi ya wagombea wa nafasi hizo utakuwa mgumu sana kwao.
Baadhi watapoteza maisha, baadhi wataumizwa, baadhi watatajirika na baadhi watafirisika.
Ni mwaka ambao watu wa nyikani hatupendi ufike haraka, ingawa majira na nyakati zipo chini ya Mungu mwenyewe, anaendelea kuufanya usiku na mchana na hatimaye tunasogea katika daraja la mwaka huo 2015 na tayari baadhi ya watu wameanza kukunja suruali ili wavuke.
Fitina zimeanza za kuwekeana miba njiani ili wenzao wasifikie mwaka huo na kila mmoja kwa dhamira yake anafanya ajualo.
Ole wao waandishi wa habari wenye misimamo ya kitaaluma. Ole wao waandishi wa habari wenye misimamo ya njaa na kupenda kuhongwa na wagombea ili kuwachafua wagombea wengine.
Ole wao waandishi wa habari ambao hawataweza kuonesha misimamo yao kuwa wa moto au baridi.
Ole wao ambao hawajui kuwa ole hizi ni zao mwaka 2015, kipindi ambacho wanasiasa wengi wataingia kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya U-Rais, ubunge na udiwani, jambo ambalo litazua hekaheka nchini.
Nasisitiza kuwa ole wao, maana najua kila mwaka wa uchaguzi wengi wanatumika kama madaraja ya kuwavusha wanasiasa, wanatumika kama makalai ya kujengea ghorofa, kisha baadae wanaonekana kama takataka.
Hakuna anayejali kuwatumia baadhi ya waandishi wa habari hata kwenye fitina za kisiasa na hakuna anayejali kuona waandishi wanauawa au kuumizwa na wanasiasa kipindi cha uchaguzi, ndiyo maana nasema kuwa ole wao waandishi wa habari.
Mbali na wanataaluma hao ambao sasa wanatakiwa kuzijua ole hizi, pia wanasiasa hasa wale ambao watajiingiza kwenye vinyang’anyiro vya nafasi hizo kuanzia ndani ya chama na katika chaguzi za serikali wakiwakilisha vyama vyao, nao pia nawahurumia.
Ole wao wanasiasa hao, kwa kuwa hakuna ubishi kuwa wao kwa wao hawapendani hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Ole wao kwasababu baadhi watakamatwa na kuwekwa mahabusu na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), huku baadhi wakipelekwa mahakamani na baada ya uchaguzi kuisha, wataonekana kuwa hawana hatia.
Ole wao kwa maana baadhi yao watasingiziwa hata mambo ambayo hawajawahi hata kuyawaza sirini wala hadharani ili tu wale watakao kuwa na mtandao mkubwa washinde, potelea mbali fitina hizo hata zikipitia chama kingine.
Ole wao endapo hawataweza kujihadhali na kuzishika ole hizi kama tahadhali kwao.
Waandishi wa habari na wanasiasa watakaojiingiza kwenye kugombea nafasi hizo mwaka 2015, nawapa ole endapo watatafuta pesa badala ya utu kisha wakabaki kufikiri kwa msaada wa watu wa marekani badala ya kuwa na fikra zao wenyewe.
Juma lililopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwa mkoani Mwanza, imeelezwa kuwa alikutana na baadhi ya makatibu na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM(NEC), wa kanda ya ziwa.
Akawaeleza nia yake ya kwamba amejitathini na kwamba anafaa kuwa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete Ikulu, huku akitoa sababu kuwa yeye ni kiongozi safi na aliyeishi kwa muda mrefu Ikulu.
Mwisho akatoa nauli kwa aliokutana nao ambayo baadhi waliitafsiri kuwa ni rushwa.
Siamini kama ilikuwa rushwa, bali naamini kuwa ilikuwa ni posho kwasababu wengi tumewahi kupata posho tunapoketi na wakubwa wa namna ya Pinda, hasa sisi waandishi wa habari.
Waziri Mkuu Pinda, aling’ara sana alipokuwa Waziri wa Tamisemi, lakini alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, kasi yake iliyozoeleka na matumaini kwa watanzania dhidi yake yakafifia.
Pinda huyu anayetaka kuwa Rais, ni yule aliyewahi kutoa machozi pale Bungeni baada ya kubanwa na hoja za mauaji ya Albino.
Pinda huyu, ni yule aliyewahi kusema kuwa ‘’tumechoka sasa, wanaokaidi amri wapigwe tu’’.
Watu wa nyikani wanasema kuwa kiongozi huyu anafaa kuwa Rais, lakini siyo kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM). Katika maelezo ya waliomnukuu, hawajagusia kwamba Pinda, alizungumza jambo lolote kuhusu chama chao.
Watu wa nyikani tunajiuliza, hivi kweli Pinda huyu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali, ataweza kuwaambia nini wananchi hasa wakulima wa Pamba katika Nyika ya Shinyanga ambao walilazimishwa na serikali kununua mbegu za pamba ambazo hazikuota na Mawaziri wake kusema kuwa serikali haitawalipa fidia?
Wakulima hawa wanaitazamaje serikali, akiwemo Waziri Mkuu Pinda na CCM yake?
Pinda huyu atawaeleza nini wananchi wa Kiteto ambako kulitokea mauaji ya Mchungaji wa kanisa kuchinjwa?
Pinda huyu atawaeleza nini watanzania ambao walipigwa katika oparesheni tokomeza majangili na kulazimishwa kufanya ngono na miti mbele ya umbu za viuno vyao? Je hawa wana amani na CCM pamoja na pinda kiongozi ambaye ndiye mtendaji mkuu wa serikali?
Pinda huyu atawaeleza nini watanzania ambao kwa sasa wakienda katika ofisi za umma kupata huduma bila rushwa hawapati? Imekuwa kama mfumo rasmi wa serikali?
Hawa na wengine wengi, wanafikiri nini kuhusu Pinda, CCM na Rais Kikwete?
Waziri Mkuu Pinda anafaa kuwa Rais, lakini siyo kupitia CCM, akihamia chama kingine atawaambia watanzania kuwa alikuwa akishindwa kuchukua hatua kutokana na mfumo wa CCM na Rais Jakaya Kikwete hakuwa tayari kuona maamuzi magumu.
Santuli ya Pinda ni nzuri ingawa haina kibwagizo, naupenda mkoa wa Mwanza, maana hata January Makamba na Edward Lowassa nao walitangazia huko uzinduzi wa santuli zao za matumaini.
Mwandishi 0754 440749
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment