KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad Slaa,
amezungumzia migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali
nchini na kusababisha mauaji ya kutisha, akisema italiweka pabaya taifa
na hivyo kumshauri Rais Jakaya Kikwete, amfukuze kazi Mkuu wa Wilaya ya
Kiteto, vinginevyo wananchi wanaoona damu ikimwagika hawawezi kumwelewa.
Dk. Slaa pia
aliwataka Watanzania wote hususani jamii za wakulima na wafugaji kuacha
kupigana na kuuana wakigombea ardhi badala yake waiwajibishe Serikali
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa migogoro hiyo ni matokeo ya
serikali hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hasa katika kuweka mipango
mizuri ya matumizi ya ardhi ambayo ni majukumu ya Serikali za Mitaa.
Dk. Slaa
alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya chama
hicho iliyopewa jina la ‘Operesheni Delete CCM’ akimpokea Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyezunguka mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na
Morogoro.
Alisema kuwa
migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na
kusababisha umwagaji damu za Watanzania na uharibifu mkubwa wa mali ni
matokeo ya kushindwa kwa sera, mipango na mikakati ya CCM, hivyo
akawataka wananchi kujiandaa kukipumzisha chama hicho kutoka madarakani.
Akizungumza
katika mkutano wake wa kwanza kijijini Mvuha, kati ya mikutano mitano
kwenye vijiji mbalimbali vya majimbo ya Morogoro Kusini, Morogoro
Kaskazini na Kilosa, Dk. Slaa alisema kuwa umwagikaji wa damu huo
usipodhibitiwa na migogoro hiyo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, serikali
itakuwa imeshindwa moja ya majukumu yake ya msingi ya kulinda raia wake.
“Ndugu
zangu, ziara hii itanifikisha katika maeneo ambayo mnajua yamekuwa na
migogoro ya ardhi…kumekuwepo na migogoro hata huku kwenu isiyokwisha ya
wakulima na wafugaji kugombea ardhi…Mkoa wa Morogoro baraka ya ardhi na
utajiri wa rutuba mliopewa umekuwa ukigeuka laana kiasi cha damu za watu
kumwagika.
“Yanatokea
sana huko Mvomero, Kilosa hata hapa kwenu (Mvuha) nimeambiwa migogoro
ipo. Tunavyozungumza hivi sasa kuna matukio ya kutisha yametokea huko
Kiteto, Siha, Malinyi na kwingine. Ndugu zangu, wakulima na
wafugaji…ninyi wote ni Watanzania. Nawaomba sana muendelee kuishi kama
ndugu kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema.
Dk. Slaa
aliongeza kuwa hayo ni matokeo ya serikali kushindwa majukumu yake na
vile vile kushindwa kwa sera za CCM, mipango na matumizi mazuri ya
ardhi.
Alisema kuwa
ili ardhi ya mifugo na kilimo ijulikane na matumizi mengine ni kazi za
Serikali za Mitaa kupitia halmashauri, hivyo akawasihi wananchi kuwa
huko kote sera za CCM zimeshindwa, kwamba ndio maana wanasema ‘delete
CCM’.
“Kupitia
mkutano wangu huu leo tunaitaka serikali ya Kikwete ichukue hatua za
haraka sana kuzuia umwagaji wa damu unaoendelea na kutafuta ufumbuzi wa
kudumu wa migogoro ya ardhi nchini. Vinginevyo wanazidi kudhihirisha
kuwa wamechoka na watakiwa kupumzishwa.
“Kwa Kiteto
mojawapo ya chanzo cha mauaji yanayoendelea huko ni wanasiasa
wanaoongoza wilayani humo, akiwemo Mkuu wa Wilaya, yuko Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya, yupo mbunge wa jimbo ambaye amewahi kuwa
waziri…mgawanyo wa ardhi ni jukumu la serikali. Hatuwezi kuangalia tu
damu ya Watanzania inamwagika kama kuku. Hatuwezi. Tunamtaka Kikwete
amfukuze kazi huyo DC,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza
kuwa iwapo viongozi walioko madarakani sasa hawataona thamani za damu
zinazomwagika kwa sababu ya wao kushindwa kutekeleza wajibu wao, iko
siku watailipa kwa gharama kubwa endapo wananchi wataendelea kupoteza
matumaini huku haki ikiwa haipatikani, huku akisisitiza kuwa hayo
yataanza kuonekana kuanzia uchaguzi wa Desemba 14 mwaka huu.
Dk. Slaa
ambaye jana alifanya mikutano katika vijiji vya Mvuha, Kisika, Ludewa,
Magubike na akimaliza mkoa wa Morogoro akiingia mkoani Dodoma leo,
aliwataka Watanzania katika jamii zao, zikiwemo za wakulima na wafugaji,
kuacha kuuana wao kwa wao, badala yake wajue namna ya kushughulikia
chanzo cha migogoro yao.
IGP aongeza nguvu Kiteto
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi
ya askari katika kijiji cha Chekanao, Kata ya Kiperesa wilayani Kiteto
mkoani Manyara kufuatia wananchi katika kijiji hicho kujitolea nyumba
kwa ajili ya kuishi askari kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo
yao kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa
mauaji.
IGP Mangu
aliyasema hayo jana wakati alipokuwa katika ziara wilayani humo ya
kujionea uharibifu uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro
hiyo iliyopelekea kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi
karibuni ambapo watu kadhaa wanashikiliwa kutokana na vurugu hizo.
Alisema
kufuatia kuwepo kwa umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho,
atahakikisha askari wa kudumu wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi
katika kuwabaini wahalifu wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo
ambapo wananchi nao waliahidi kujenga kituo cha polisi.
Mtendaji wa
Kijiji cha Chekanao, Omar Ndee alisema wamekuwa wakipata shida kutokana
na umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo ambalo limekuwa likifanya
kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na migogoro ya ardhi
katika wilaya ya Kiteto.
Watu 16 mbaroni
Katika hatua
nyingine, watu 16 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kufuatia vurugu kubwa
zilizozuka za kugombea eneo la malisho katika kijiji cha Miti Mirefu,
Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baina ya jamii ya kifugaji ya
Kimaasai na mwekezaji wa shamba la Ndarakwai.
Akithibitisha
tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema
waliokamatwa jana kufuatia oparesheni ya jeshi la polisi ni jamii ya
wafugaji.
Gama alisema
kati yao wanaume ni 11 na wanawake watano waliokutwa na vifaa vya
mwekezaji kama kompyuta mpakato (laptop), magodoro, vitanda, meza na
vitu vingine vya thamani.
Mwishoni mwa
wiki iliyopita watu wanaodaiwa kuwa jamii ya kifugaji, walilivamia
shamba la mwekezaji huyo, ambaye pia anafanya utalii wa picha, kambi za
watalii na kufuga wanyama na kusababisha vurugu ambazo zilizuka baada ya
mifugo zaidi ya 300 ya jamii ya wafugaji wa Kimaasai kutoka wilaya ya
Longido na nchi jirani ya Kenya, kudaiwa kuingiza mifugo yao kwenye
shamba la mwekezaji huyo baada ya kukosa eneo la malisho ya mifugo yao
ambapo magari na nyumba viliteketezwa kwa moto.
CREDIT: TANZANIA DAIMA
0 maoni:
Post a Comment