LEO NI MIAKA 25 YA KUANGUKA KWA UKUTA WA BERLIN, HOFU YA VITA BARIDI BADO YATANDA
Ujerumani leo hii inaazimisha miaka 25 ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin huku ikirusha maputo 8,000 kwenye mstari wenye urefu wa maili tisa (kilometa 13.5) mahali ambako zamani palijengwa ukuta huo kutenganisha Mashariki na Magharibi.
Mabaluni hayo yatarushwa majira ya saa 1.18 usiku (saa 4.18 kwa saa za Afrika Mashariki) ili kusherehekea wakati wananchi wa Ujerumani Mashariki walipoanza kukwea ukuta huo na kuingia Magharibi mnamo Alhamisi Novemba 9, 1989.
Ukuta huo ulijengwa Berlin Magharibi mwaka 1961 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (GDR-Ujerumani Mashariki), kupinga utawala wa kifasishti.
Lengo kubwa la kujengwa kwa Ukuta huo lilikuwa kuzuia wananchi wa Mashariki kwenda magharibi.
Katika kipindi chote cha miaka 28, Ukuta wa Berlin ulikuwa alama muhimu ya Vita Baridi ukiwa na minara ya ulinzi pamoja na "nyaya za kifo" ambapo takriban watu 5,000 walipoteza maisha yao wakijaribu kukimbia utawa wa mabavu.
Lakini nyufa zilianza kuonekana wakati wa mapinduzi yasiyo ya damu yalipotokea Poland na Hungary na kulegeza mfumo wa kikomunisti wa Ulaya Mashariki.
Mahitaji ya sera za uwazi (glasnost) na marekebisho (perestroika) ya kiongozi wa Soviet Mikhail Gorbachev ndiyo yaliyoleteleza matukio hayo ya kihistoria.
Gorbachev (83) hivi sasa yuko jijini Berlin kushiriki sherehe hizo za robo karne ambazo zitahusisha matamasha huko Brandenburg Gate na uzinduzi wa makumbusho ya Ukuta.
Lakini Gorbachev ameonya kwamba ulimwengu umeshindwa kujifunza madhira ya uadui ambao uliigawa Ulaya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Akirejea hali ya sasa kati ya Magharibi na uamuzi wa Rais wa Russia Vladimir Putin nchini Ukraine, alisema: "Dunia iko katika hatari ya Vita Baridi mpya. Baadhi tayari wamesema kwamba imekwishaanza."
Chancellor wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alizaliwa Hamburg lakini akakulia mashariki, ataongoza maazimisho ya leo kwa kuhutubia kwenye Makumbusho ya Ukuta wa Berlin.
Huko nyuma alikwishawahi kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kuvunjika kwa Ukuta huo kwa raia wa Ujerumani.
"Hata leo ninapotembea kupita Geti la Brandenburg, bado kuna hisia kwamba hili lisingewezekana kwa miaka mingi katika maisha yangu, na kwamba nililazimika kusubiri kwa miaka 35 kupata hisia hizi za uhuru," alisema Merkel wiki iliyopita.
"Hiyo ilibadili maisha yangu," akaongeza.
Muungano wa Ujerumani ulichukua takriban mwaka mmoja kukamilika baada ya kuanguka kwa Ukuta na tangu hapo takriban Euro 2 trilioni zimetumika kujaribu kurekebisha mambo.
Ujerumani imepanda na kuwa taifa tajiri na lenye ushawishi mkubwa barani Ulaya.
Hata hivyo, bado hakuna usawa: ukosefu wa ajira ni mkubwa mashariki, wakati uzalishaji wa viwandani umeongezeka zaidi magharibi.
0 maoni:
Post a Comment