Na Peter Elias, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakazi
wa Jiji la Dar es Salaam sasa wataanza kusafiri kwa kutumia kivuko cha
kisasa kutoka katikati ya jiji hadi Bagamoyo na mikoa mingine badala ya
kutumia usafiri wa barabara.
Kivuko hicho
kilichopewa jina la MV Dar es Salaam, kimeletwa nchini jana kutoka
Bangladesh kikiwa cha kwanza kwa mwendokasi kuliko vingine vyote nchini.
Kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa pamoja na mizigo.
Akizungumza
katika hafla ya kupokea kivuko hicho kwenye Bandari ya Dar es Salaam,
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuri alisema ujio wa kivuko hicho chenye
thamani ya Sh7.9 bilioni ni mwanzo wa utatuzi wa kero ya foleni katika
jiji hili.
Dk magufuli
alisema kumekuwa na utegemezi mkubwa wa usafirishaji kwa njia ya
barabara, jambo ambalo linasababisha foleni bila sababu ya msingi.
“Asilimia 99
ya mizigo husafirishwa kwa njia ya barabara, wakati asilimia moja tu
ikisafirishwa kwa ndege, treni na meli. Hakuna haja ya kusafirisha
makontena kwa njia ya barabara, tunahitaji usafiri wa treni kusafirisha
makontena kutoka bandarini kwenda nje ya mji ili malori yakapakie huko,”
alisema.
Alisema kwa
kufanya hivyo kutasaidia kupunguza adha ya foleni, ambayo mara nyingi
husababishwa na malori yanayobeba mizigo kutoka au kwenda bandarini,
hasa katika Barabara za Mandela na Kilwa.
Waziri huyo
alibainisha miradi mingine ya kupunguza foleni itakayotekelezwa jijini
ni ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo
na Tazara. Pia, ujenzi wa Daraja la Kigamboni litakalokamilika Juni,
mwakani na kugharimu Sh214 bilioni.
Alisema
mradi mwingine wa Mabasi Yaendayo Kasi (BRT) utagharimu Sh288 bilioni na
unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani. Alibainisha kuwa bado ujenzi wa
barabara za mzunguko unaendelea na kumtaka mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
kudhibiti wafanyabiashara ndogondogo wanaoingilia hifadhi ya barabara
na kusababisha foleni.
“Dar es Salaam inahitaji vivuko vingine vingi zaidi, tuna Sh3.7 bilioni kwa ajili ya kivuko kingine cha Dar es Salaam,” alisema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Mhandisi
Marcellin Magesa alisema mradi wa ujenzi wa kivuko cha Dar es Salaam –
Bagamoyo ulianzishwa na Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2013/14.
CREDIT: MWANANCHI
0 maoni:
Post a Comment