WAGONJWA WA MALARIA SASA WAPIMWA KWA MACHO!


Na Beatrice Shayo, Nachingwea
Ukosefu wa vifaa tiba katika baadhi ya zahanati na vituo vya afya vya Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, umewalazimu wauguzi wa vituo hivyo kuwatibu wagonjwa wa malaria kwa kutumia uzoefu wa kuwaangalia.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika zahanati ya Mtepeche kata ya Kilimani Hewa, tarafa ya Nambambo na zahanati ya Kihuwe kata ya Naipingo, tarafa ya Naipanga wilaya ya Nachingwea, umebaini kuwepo kwa tatizo hilo.

Waganga wa zahanati hizo, walisema kukosekana kwa vipimo vya kupimia ugonjwa wa malaria kunawalazimu kutibia wagonjwa kwa kutumia uzoefu wa kuwaangalia kwa macho.

Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mtepeche, Ibrahimu Mpini, alisema hutumia uzoefu kwa kumwaangalia mgonjwa kwa macho na kumpatia huduma.
Alisema njia hiyo ni hatari kwa kuwa unaweza kutoa dawa za malaria wakati mgonjwa ana tatizo hilo.

Alisema ukosefu wa vipimo ni changamoto katika utendaji kazi wao.
Hata hivyo, alisema wamekuwa wakiomba vifaa hivyo kwenye Bohari ya Madawa (MSD) lakini wanapata vichache ukilinganisha na mahitaji yao.

Alisema MSD huwapatia vifaa hivyo kila baada ya miezi mitatu na wakati mwingine havifiki muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kihuwe, Rajabu Nassor, alisema  kituo chake kinapa idadi ndogo ya vifaa vya  kupimia malaria.

Alisema kutokana na uchache huo huwa vinaisha katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu wakati MSD hupita kila baada ya miezi mitatu.

Nassor alisema wanachokiandika na kile kinachotolewa na MSD ni tofauti, hivyo kuna umuhimu wa jambo hilo kuangaliwa kwani kuwatibu wagonjwa kwa macho si jambo zuri kiafya.

Alisema zahanati yake inawatibia wagonjwa kutoka katika kata tano na vifaa hivyo vinapokwisha mapema inawalazimu kufanyakazi katika mazingira magumu.

Aliishauri serikali kuhakikisha zahanati hizo zinakuwa na vifaa muhimu ili wananchi hao wasipate usumbufu wa kupata huduma za afya.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment