Ikulu sasa yafuta ulaji Krismasi, Mwaka Mpya.
Hatua za kupunguza gharama za matumizi ya serikali chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli, ili kuboresha huduma za jamii zimeendelea kushika kasi jana baada ya Ofisi ya Rais, Ikulu kupiga marufuku matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya uchapishaji wa kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya
Krismasi husherehekewa Desemba 25 na Mwaka Mpya Januari mosi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, alitangaza hayo jana ikiwa ni hatua mojawapo ya kuongeza nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Kadhalika, Balozi Sefue ameagiza kuwa fedha zilizopangwa kugharimia utengenezeji na uchapishaji wa kadi, zitumike kupunguza madeni yanayozikabili wizara, idara, taasisi na mashirika mbalimbali ya umma, kwa kuhakikisha kuwa wanawalipa wananchi ama wazabuni waliotoa huduma na bidhaa mbalimbali kwao au kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapelekwa kwenye matumizi mengine ya vipaumbele vya taasisi husika. Balozi Sefue alifafanua kuwa kadi hizo ni zile ambazo hutolewa na wizara, ofisi za wakuu wa mikoa, ofisi za wakuu wa wilaya na taasisi mbalimbali za umma kwa ajili ya kupeana salamu ya sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya na wakati mwingine kuambatanishwa na zawadi.
Taarifa hiyo ya Balozi Sefue iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Balozi Sefue amefafanua kuwa yeyote ambaye atataka kutengeneza ama kuchapisha kadi hizo, basi atimize dhamira hiyo kwa gharama zake na siyo kwa fedha za serikali.
Uamuzi huo wa Balozi Sefue ni muendelezo wa hatua za serikali ya awamu ya tano kupiga marufuku matumizi holela ya fedha za umma.
Kabla ya hatua hiyo jana, Rais Dk. Magufuli alishatangaza kupiga marufuku safari holela za nje, kufuta maadhimisho ya sherehe za Uhuru ambazo hufanyika Desemba 9, kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyopaswa kufanyika kitaifa Desemba Mosi mkoani Singida na pia tayari alishatangaza mara kadhaa kuwa kamwe serikali yake haitaruhusu maadhimisho ya Wiki ya Maji na mengine kama hayo kwani mara zote hutoa mianya ya wizi wa fedha za serikali.
Uchapishaji wa kadi za sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya na pia sikukuu nyinginezo unatajwa kuwa ni moja ya maeneo yanayotumiwa na baadhi ya maofisa wa serikali wasio waaminifu kujinufaisha binafsi kwa kugeuza siku hizo kuwa ni ‘ulaji’ kwao kupitia gharama kubwa wanazoonyesha bila kujali uhalisia wa bei.
CHANZO: NIPASHE
from Blogger http://ift.tt/1Yx6hQV
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment