SHERIA YA MANUNUZI YAFUMULIWA NA RAIS DR MAGUFULI


Magufuli afumua Sheria Manunuzi

TUME ya Kurekebisha Sheria imeanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 kama njia ya kuitikia mwito wa Rais John Magufuli ambaye aliahidi kuifanyia marekebisho sheria hiyo wakati analizindua Bunge la 11.

Tayari Tume hiyo imetoa tangazo linalowataka wananchi au taasisi mbalimbali kutoa maoni ndani ya siku 30 kuanzia jana. Maoni na mapendekezo hayo yanaweza kuwa ya jumla au kuhusu masharti mahususi ya sheria au mifumo ya kitaasisi iliyoundwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Akilihutubia Bunge, katika eneo la kuziba mianya ya rushwa, Dk Magufuli aliahidi kuifumua sheria hiyo ambayo inatoa mianya kwa watumishi wa umma kuiba fedha za umma. “Tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba.

Ni matarajio yangu tutakapoleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono,” Dk Magufuli alisema katika hotuba hiyo.

Kwa mujibu wa tangazo la Tume hiyo, madhumuni ya utafiti huo ni kubainisha upungufu katika utekelezaji wa sheria, kubainisha madhara ya upungufu huo katika utekelezaji wa sheria kwa Serikali na taasisi zake.

Tume hiyo imeainisha maoni hayo kuhusu misingi ya soko, pamoja na mabadiliko endelevu ya kisheria, hatua mbalimbali katika mchakato wa ununuzi wa bidhaa au huduma, ulinganifu wa thamani ya fedha kwa bidhaa inayonunuliwa au huduma inayotolewa.

Maoni mengine ambayo Tume hiyo inaomba kutoka kwa wadau ni kuhusu mgogoro unaojitokeza katika sheria zinazohusiana na ununuzi wa umma na athari za kibinadamu katika mchakato wa ununuzi kama vile rushwa, mgongano wa maslahi binafsi na ukosefu wa maadili.

Sheria ya Ununuzi wa Umma inayotumika sasa ilitungwa na Bunge mwaka 2004 na kufanyiwa marekebisho makubwa na Bunge mwaka 2011 kwa lengo la kuweka mfumo wa kisheria na kitaasisi wa usimamizi wa ununuzi wa umma.

Katika utekelezaji wa sheria hio, Serikali na taasisi zake zimebaini kasoro ambazo zimekuwa kikwazo katika utekelezaji bora wa sheria hiyo tangu ilipotungwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001.

Kasoro zimeendelea kuwepo hata baada ya Bunge kuifuta na kutungwa upya Sheria ya Ununuzi wa Umma mwaka 2004. Miongoni mwa kasoro hizo ni pamoja na mlolongo mrefu na gharama nyingi katika mchakato wa ununuzi kabla ya kufanya ununuzi unaokusudiwa.

Chini ya sheria hiyo, Serikali imekuwa inauziwa bidhaa mbalimbali kwa bei kubwa tofauti na bei halisi ya soko jambo ambalo limeifanya Serikali kutumia fedha nyingi kwenye manunuzi. Kwa mujibu wa Bodi ya Manunuzi ya Umma, Serikali inatumia asilimia 70 ya bajeti yake kwa ajili ya kufanya manunuzi mbalimbali.

Pia sheria hiyo inatoa mianya kwa baadhi ya maofisa wa Serikali kufisadi fedha za umma na kusababisha hasara ya mabilioni ya fedha. Udhaifu mkubwa katika sheria hiyo ni pale Serikali inapotakiwa kulipia riba katika ununuzi wa bidhaa mbalimbali jambo ambalo limekuwa linaigharimu serikali fedha nyingi.

Miongoni mwa mapungufu ya sheria hiyo ni adhabu zinazotolewa kwa watu wanaoisababishia hasara Serikali ambayo kwa mujibu wa sheria hiyo, anatakiwa kufungwa jela kifungo kisichopungua miaka saba na kulipa faini isiyopungua Sh milioni 10.


HABARI LEO

from Blogger http://ift.tt/1O8c6TF
via IFTTT


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment