Kwa Msaada wa Daily Mail.
Mwaka mmoja una siku 365, siku ambazo
zinaweza kuwa na mabadiliko kwa kiasi kikubwa, siku ambazo jua linazama,
linachwea, kunatokea mvua kisha kiangazi. Mojawapo ya wanaoweza kuwa na
simulizi ya kusisimua juu ya utofauti huu ni klabu ya Chelsea na
mashabiki wake.
Miezi 12 kamili iliyopita kama leo,
Chelsea walikuwa chini ya Kocha Jose Mourinho akishuhudia wakipoteza
mchezo nyumbani kwa Leicester City ikiwa ni moja kati ya viwango vibovu
vya bingwa mtetezi. Hii ilimaanisha kuwa mmiliki wa klabu hiyo, Roman
Abramovich alikuwa amekula na kuvimbiwa, hakuhitaji tena ladha ya
chakula anachopika Jose Mourinho, na wiki hiyo alimtimua.
Kumbukumbu mbaya sana lakini katika siku
nzuri kama ukiamua kulinganisha ama kufananisha. Jaribu kufikiri mkosi
ule na Chelsea ya Leo, wapo katika nafasi ya kwanza, wanaongoza kwa
pointi sita na wanao uhakika wa kuongoza mpaka kipindi cha Christmas,
huku pia rekodi zikionyesha kuwa katika mara nne zilizopita ambazo
waliongoza mpaka wakati wa Christmas, walimaliza kwa kuwa mabingwa.
Hiki ni kipindi cha Keki na Mvinyo kwao,
sherehe na matarumbeta, vigeregere na vifijo. Hakuna wa kuwazuia kuwa
hivyo, na kile ambacho Mourinho alikifanya kionekane kigumu Antonio
Conte anakifanya kiwe rahisi. Ushindi dhidi ya Sunderland ulikuwa ni wa
kumi mfululizo kwao, na kama wakipata ushindi mara tano mfululizo
watakuwa wanaweka rekodi yao mpya wakivunja ile ya Arsenal ya mwaka
2002.
Hata Antonio Conte amegusia na kusema: Ni
raha iliyoje kushinda michezo 10 mfululizo kwenye ligi hii, kwa sababu
ni ngumu mno. Inabidi kupigana katika kila mchezo, wachezaji wetu
wanastahili hili kutokana na kujituma kwao na nguvu kazi yao kila siku
kwenye michezo tunayohusika.
Lakini sipendi kutizama msimamo wa ligi kwani ligi haijamalizika leo.’
Inaonekana kabisa kuwa kuna utulivu na
mamlaka kwa upande wa Conte, kama ilivyokuwa kwa klabu na wachezaji
anaowaongoza. Huku Mourinho hakiwa aliyekuwa amepoteza mamlaka ya vyumba
vya kubadili nguo, Muitaliano huyu ameweza kuwafanya wachezaji wake
wote kucheza katika kiwango ambacho hakuna aliyekiona msimu uliopita.
Anathubutu hata kuwaruhusu kunywa bia
kiasi baada ya kila mchezo, ukaribu wao ni mkubwa na mafanikio yao mpaka
sasa ni kama yamewalevya mashabiki.
Naam, tukizingumzia kila mchezaji kuwepo
anapohitajika ni kama walivyohitaji kipa wao Thibaut Courtois kufanya
kazi kubwa kuokoa mpira uliopigwa na Patrick van Aanholt katika dakika
za mwisho ambao ungeweza kumaanisha wametoka sare.
Cesc Fabregas alikuwa ni moja kati ya
wachezaji ambao hawakuwa kwenye maelewano na Jose Mourinho huku pia
akianza msimu akiwa benchi lakini katika mara zote alizohitajika
amefanya vyema huku pia akiwa mfungaji wa bao la ushindi dhidi ya
Sunderland.
‘Nina furaha kubwa na Cesc,’
alisema Conte. ‘Ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengine. Pamoja na kuwa
ni mara ya tatu pekee anaanza msimu huu, lakini amekuwa ni mtu mwenye
kujituma kwa kiasi kikubwa.’
Kwa upande wa Sunderland na David Moyes,
bahati mbaya ipo upande wao kwani hii inakuwa ni mara ya 11 wanapoteza
huku pia ikija baada ya kocha huyo kufanya mazungumzo na mtendaji wa
klabu hiyo Martin Bain ambaye alimwambia kuwa klabu haitojaribu
kujinasua kutoka mkiani kwa kuingia sokoni mwezi Januari.
Kauli iliyomkera kocha huyo kwa kiasi kikubwa.
Huu ni muda wa Chelsea, ni wakati wao, wanaweza kunywa wanavyotaka,
wanaweza kushangilia kwa nafasi yao, waruke watakavyojisikia kwa
sababu wana kila keki wanayotaka na visu vipo mikononi mwao. Kikubwa ni
kutokulala kwenye sherehe, wataibiwa.
0 maoni:
Post a Comment