ZITTO KABWE: BUNGE LINAPASWA KUILINDA HADHI YAKE

Hoja ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliyoitoa Februari 9 mwaka huu, Bungeni mjini Dodoma:
Kwa mujibu wa kanuni ya 51, kanuni ndogo ya 51(1) mpaka 51(4), jambo hilo linaihusu Mamlaka ya Jeshi la Polisi kukamata waheshimiwa Wabunge wakati mikutano ya Bunge lako tukufu inaendelea.
Tunafahamu kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge , sheria hiyo imezuia Mbunge yeyote kukamatwa ndani ya viunga vya Bunge isipokuwa tu kwa ruhusa ambayo imetolewa na Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na si hivyo tu, nilikwenda kwenye maktaba ya Bunge katika kujaribu kuangalia mwenendo wa mabunge mengine ya Jumuia ya Madola. Kama unavyofahamu , licha ya kuongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni za Bunge na maamuzi ya maspika waliopita, pia Bunge letu kama sehemu ya Jumuiya ya Madola, linaongozwa kwa taratizu za Jumuiya ya Madola na maamuzi ambayo yamefanywa na mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola.
Ninacho kitabu cha Erskine May ambacho ndio ‘msahafu’ (kitabu kikuu cha rejea) wa taratibu za mabunge ulimwenguni na kimeeleza katika sehemu yake ya 14 kuhusiana na ‘Criminal Law & Statutory Detention, house to be informed of arrests’, kwamba Bunge linapaswa kujulishwa juu ya dhamira ya kumkamata Mbunge. Na kitabu hicho kinafafanua na kutoa mifano ya dhahiri ya mabunge mbalimbali ya Jumuiya ya Madola juu ya taratibu mbalimbali zinazotumika pale ambapo Mbunge anatakiwa kukamatwa na mamlaka nyengine katika nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola.
Tuna matukio kadhaa hapa ambayo yametokea, tukio la kwanza ni la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema. Alikuja Bungeni, akashiriki kwenye shughuli za Bunge lakini alipotoka akakamatwa, akaenda kushtakiwa jijini Arusha. Kwa taratibu halali kabisa za kisheria, lakini mpaka leo hivi tunavyozungumza, Bunge lako halina taarifa rasmi yoyote juu ya kama ukamataji wake ulifuata taratibu ambazo zimeelezwa na Sheria yetu ya Kinga na Madaraka ya Bunge pamoja na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Lakini pili, taratibu za mabunge zinaeleza kwamba, hata kama Mbunge amekamatwa, kokote kule, kwa kosa lolote lile, baada ya kuwa amekamatwa, mamlaka zilizomkamata ama Hakimu au Jeshi la Polisi, wanapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa Bunge juu ya ukamataji husika, na taarifa ile Spika wa Bunge aisome ndani ya Bunge kuwataarifu wabunge, ni kwa nini Mbunge mwenzao hayupo kwenye shughuli za Bunge. Hadi sasa hakuna taarifa yoyote ambayo imetolewa kwa ajili ya kuelezea juu ya kukamatwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini ambaye mpaka sasa bado yupo mahabusu na kesi yake ikiendelea. Lakini tuna Mbunge ambaye amefungwa, amehukumiwa kifungu cha miezi sita jela, Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero. Kwa taratibu na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola, ilipaswa Hakimu atoe taarifa rasmi kwa Spika wa Bunge kumjulisha juu ya suala hilo.
Kwa sababu katika matukio yote haya ya nyuma , Bunge letu limeshindwa kuchukua hatua zozote juu ya kuhakikisha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge imetekelezwa, Jeshi la Polisi sasa limeona hiyo ni kawaida.
Si hilo tu, Februari 6 mwaka huu, Mbunge wa Singida Mashariki, ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, wakati akitoka nje ya geti la Bunge alikamatwa. Kwa maana hiyo ni kwamba, Tundu Lissu alikamatwa si tu bila ya ‘approval’ (ridhaa) ya Spika wa Bunge, bali hata angalau kumwandikia ujumbe mfupi wa simu Spika wa Bunge kwamba tunamkamata Mbunge wako.
Mihimili yote ya dola inalinda hadhi yake kwa wivu wa hali ya juu, mihimili wa Bunge umechezewa mno na haujilindi, hauchukui hatua zozote za kulinda hadhi yake. Kwakuwa jambo hili linaihusu haki za Bunge, ni jambo ambalo linapaswa kujadiliwa na kutolewa ‘resolution’ (maazimio) na Bunge. Na hali hiyo si jambo jipya, huko nyuma tumeshawahi kuwa na Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, alikamatwa mwaka 2011 huko jimboni kwake Mbarali, bahati nzuri Spika Anna Makinda alikuwa analinda hadhi ya Bunge kwa namna yoyote ile, alitolewa yule Mbunge.
Pia alikamatwa Mbunge wa lililokuwa Jimbo la Nzega (kabla Nzega haijagwanywa na kuwa majimbo mawili ya Nzega Mjini na Nzega Vijijini), Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akizuia kufungwa kwa migodi ya wachimbaji wadogo wa Mwashina yaliyo jirani na mgodi wa Resolute Tanzania Limited wilayani Nzega mwaka 2014, zilifanyika juhudi maalumu za kibunge kuhakikisha Mbunge huyu anatolewa. Hii ya sasa, wabunge wanakuja ‘kunyakuliwa’ wakiwa Bungeni Dodoma, tena vikao vya Bunge vikiwa vinaendelea.
Nchini Uingereza, mwaka 2011 kulitokea jambo kama hili, ikaenda hoja kama hii ndani ya Bunge, Bunge likapitisha azimio kwamba linawekea nguvu sheria yake ya kinga, haki na madaraka ya Bunge. Kwamba Mbunge yeyote atapokuwa anataka kukamatwa kwa makosa yoyote, ni lazima kwanza mamlaka za ukamataji zipate Baraka za Spika wa Bunge.
HT: MTANZANIA

from Blogger http://ift.tt/2lKXa13
via IFTTT


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment