Tutakuwa
tunaelezea kwenye safu hii maambukizi yanayosambazwa kwa kujamiana.
Wasomaji wengi wamezoea kuyaita magonjwa ya sinaa lakini gazeti hili
linataka tubadilishe tuyaite ‘Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana
(MYKK)’ na tutaelezea kwa nini.
Wanaojua
Kizungu labda watakumbuka kuwa hapo awali tulikuwa tunaita hali hizi
‘Sexually Transmitted Diseases (STD). Ukitafsiri moja kwa moja maana
yake ni Magonjwa Yanayoambukizwa Kujamiana . Tuliacha kuyaita STD na
sasa tunayaita ‘Sexually Transmitted Infections’ (STI) yaani Maambukizi
Yanayosambazwa kwa Kujamiana.
Kuna
tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) kwa kuwa
magonjwa mengine yanasababishwa na maambukizi. Kwa hiyo tofauti kati ya
magonjwa na maambukizi ni kuwa maambukizi yanazaa magonjwa. (Tofauti
kati ya yai na kuku ni kwamba kuku anataga yai).
‘Sexually Transmitted Infection’ (STI) kwa Kiswahili cha moja kwa moja ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Sexually transmitted Diseases (STD) ni Magonjwa Yanayoambukizwa kwa Kujamiana. Utaona kuwa hapa kuna
tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) Tatizo
hapa siyo la ugonjwa tu bali ni la maambukizi. Kunaweza kukawa na
maambukizi yanayotokana na kujamiana ambayo unayaona maambukizi
yenyewe, yaani unaona wadudu ambao mtu ameambukizwa kwa kujamiana,
lakini huoni ugonjwa wenyewe. Hii inatokea wa mfano mtu anapoambukizwa
na chawa wakati wa kujamiana (chawa wa mafuzi). Unawaona chawa wenyewe lakini huoni ugonjwa.
Kwenye tatizo la UKIMWI mtu anaambukizwa na
VVU. Haya ni maambukizi. Ugonjwa hauonekani moja ka moja bali
kinachoonekana ni syndroma (dalili nyingi nyingi) inayosababishwa na
magonjwa tegemezi yanayouvamia mwili baada ya kinga ya mwili kupungua.
Maambukizi mengine kwa mfano ya kisonono na kaswende; ugonjwa
unaonekana. Kwa sababu hizi za kuwa kuna hali nyingine ambapo ugonjwa
hauonekani moja kwa moja na kwa kuwa katika hali zote kuna maambukizi
basi ikakubalika hali hizi ziitwe Maambukizi Yanayosambazwa kwa
Kujamiana (Sexually Transimitted Infections - STI) Magonjwa Yanayosambazwa kwa Kujamiana (Sexually Transimitted Diseases - STD)
Ni Maambukizi ya Sinaa (MYS) au ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)?
Ni
lazima tuwashukuru wataalamu wanaojitahidi kutafsiri maneno yetu ya
kisayansi kuyaweka kwenye lugha ya Kiswahili. Tushukuru kuwa tafsiri zao
nyingi ni sawa na rahisi kuzitumia lakini kuna tafsiri ambazo wao
wametupa kianzio ili na sisi tufikirie tuone kama zinahitaji kuboreshwa.
Moja ya tafsiri ambayo inahitaji kuboreshwa ni hii ya kuziita hali hizi
magonjwa. Tumeishatoa sababu hapo juu na kuelezea kuwa tuziite hali
hizi maambukizi na siyo magonjwa.
Ukimwi unamtesa sana mwathirika |
Kwa hiyo tuseme ni Maambukizi ya Sinaa? Sinaa linamaanyisha starehe. Ni kama tunasema kuwa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana yanatokana na sinaa,
yanatokana na starehe. Hapa tunakuwa kama tunasema kuwa haya ni
maambukizi yanatokana na kustarehe bila hata kusema ni starehe gani - ya
kunywa pombe, ya kutumia madawa ya kulevya, ya kucheza dansi na musiki -
starehe zipo nyingi. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa na Starehe ya
Kujamiana?
Ni
ukweli kuwa ukichukulia kujamiana kama starehe utapata Maambukizi
Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Yanapotokea kati ya wanandoa yanatokana na
mwanandoa mmoja au wote wawili kutokuwa waaminifu na kuchukulia
kujamiiana kama starehe.
Ni
vizuri jina la hali inayohusiana na ugonjwa unapolisikia linakueleza
mengi juu ya hali yenyewe na linakuambia hata namna ya kujikinga na hali
hiyo. Hapa ukisikia maneno matatu ya jina la hali hii ‘Maambukizi
Yanayoambukizwa kwa Kujamiana’
tayari umeishajua kuwa haya ni maambukizi; kuwa mwenzako anakuambukiza
au wewe unamwambukiza. Ukisikia yanayosambazwa unajua kuwa yanasambazwa
na siyo kwamba yanaambukizwa tu. Ukisema yanasambazwa tayari umeishasema
kuwa yanaenea haraka sana kutoka mtu hadi mtu. Ukisikia kuwa maambukizi haya yanatokana na kujamiana unaanza kujisemea ‘nijichunge sana na kujamiana ovyo ovyo.’
Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK) ni mtu kwa mtu; yaani yanatoka kwa mtu mmoja yanaenda kwa mtu mwingine. Siyo
kama ilivyo kwenye ugonjwa wa kwa mfano malaria ambao vijidudu hutoka
kwa mtu mmoja; vinaingia kwa mbu na baadaye kwa binadamu. Siyo kama wa
kichocho ambao vijidudu vinatoka kwa mtu vinaingia kwenye konokono na
baadaye vinaingia kwa mtu tena. Wataalamu wanaita hali hii ya jinsi
vijidudu vinatoka kwa mwanadamu na baadaye kumrudia tena ‘mzunguko wa
maambukizi’ ambapo kuna hatua mbali mbali.
Kwanza
kuna wadudu wenyewe kwa mfano wanaosababisha Maambukizi Yanayosambazwa
kwa Kujamiana; kuna hifadhi ya hao wadudu kwa mfano hapa anayewahifadhi
ni binadamu; halafu wadudu wanaingia kwa mtu mwingine na huyo mtu
mwingine anawapeleka tena kwa mtu mwingine. Maambukizi Yanayosambazwa
kwa Kujamiana ni ya moja kwa moja kutoka kwa mtu hadi kwa mtu mwingine.
Maambukizi ya magonjwa mengine yana mzunguko mrefu zaidi ambapo kuna
wadudu wa maambukizi, kuna hifadhi yao ambayo moja inaweza ikawa
binadamu (malaria na kichocho) au mnyama (kichaa cha mbwa); wadudu
wanatoka kwenye hifadhi wanaingia kwenye mnyama mwingine kama kwa mfano
kichocho kinaingia kwenye konokono, kinatoka huko na kuingia kwa
binadamu. Kwa kujua mzunguko huu wa vijidudu vya magonjwa inajulikana ni
wapi tuingilie ili kuuthibiti ugonjwa wenyewe. Kwa kuwa inajulikana
kuwa mzunguko wa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana ni mtu kwenda
kwa mtu; na yanaambukiza kwa kujamiana, kuyakinga haya maambukizi
kunahusu kuiangalia hali ya kujamiana na kuhakikisha mtu anajamiana na
mwenzake ambaye hana uwezekano wa kuwa na hifadhi ya Maambukizi
Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK). Kuna watu ambao wana uwezekano
zaidi wa kuwa hifadhi ya wadudu wa MYKK. Kujikinga
na maambukizi haya ni vema kutojamiana nao. Hawa ni watu wanaojamiana
na watu wengi kwa mfano malaya au hata watu wa kawaida tu mradi wewe
mwenyewe umemwangalia na kujua tabia yake. Ukishajua kuwa huyu
anajamiana na wanaume au wanawake wengi au zaidi ya mmoja unajua kuna
uwezekano kuwa yeye ni hifadhi ya MYKK.
Tumeelezea ni kwa nini maambukizi haya yaitwe Mambukizi Yanayosambazwa kwa
Kujamiana na siyo Magonjwa Yanayosambazwa wa Kujamiana (STD) au
Magonjwa ya Sinaa. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana au
kwa kizungu STI. Wiki ujayo tutataja na kuanza kuelezea aina 13 za MYKK
Tuandikie kama umeishawahi kuugua MYYK utuambie ulivyoambukizwa, ulivyotibiwa na unavyoendelea. Barua hizi, majina na simu namba ni siri. Mwandike Mhariri, P.O. Box 72321 Dar es Salaam au barua pepe bahimokahumba@yahoo.com, simu meseji 0712002188 au andika kwa hapa chini.
0 maoni:
Post a Comment