Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na timu za ushindi za wanawake (CUF) kwa upande wa Unguja, wakati akizizindua rasmi kwenye ukumbi wa Majid Kiembe samaki.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, akizungumza na timu za ushindi za wanawake (CUF) kwa upande wa Unguja, wakati akizizindua rasmi kwenye ukumbi wa Majid Kiembe samaki.
Baadhi ya wajumbe wa Timu za ushindi za wanawake wa CUF Unguja, wakifuatilia mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na vijana wa barza za CUF Kidongo chekundu na Jang’ombe Urusi, alipotembelea na kuzungumza na vijana wa barza hizo
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na vijana wa barza za CUF Kidongo chekundu na Jang’ombe Urusi, alipotembelea na kuzungumza na vijana wa barza hizo
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameipongeza Jumuiya ya akinamama wa Chama hicho kwa mwamko wanaouonesha katika kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Amesema hali hiyo ni dalili njema ya mafanikio kwa chama hicho, kwa vile wanawake ambao wanachukua asilimia kubwa ya wapiga kura wa Zanzibar, wanaonekana kuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za uchaguzi katika ngazi zote.
Maalim Seif ambaye pia ni mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, ametoa kauli hiyo wakati akizindua timu za ushindi za wanawake wa CUF kwa upande wa Unguja, katika mkutano maalum uliofanyika ukumbi wa Majid, Kiembesamaki.
Amewataka wanawake hao kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaondoka madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameelezea kutoridhishwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Benard Membe hivi karibuni inayohusu waangalizi wa uchaguzi.
Amesema sio jambo la busara kwa Waziri huyo kuanza kuwatisha waangalizi wa uchaguzi, na badala yake alipaswa kuwapa moyo waangalizi hao ili waweze kazi zao kwa uhuru na uhakika.
Hata hivyo amesema chama hicho hakitegemei nguvu ya waangalizi wa uchaguzi kupata ushindi, isipokuwa nguvu ya wananchi ambao wanaonekana kukiunga mkono chama hicho.
Mapema akisoma risala ya jumuiya hiyo, Bi. Halima Abass ameushauri uongozi wa juu wa Chama hicho kuwapa fursa akinamama kuweza kusimamia kampeni za uchaguzi huo.
Ameeleza kuwa wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa harakati za uchaguzi, na kwamba watashiriki kikamilifu katika kampeni ili kuhakikisha kuwa wanapata mabadiliko ya uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej, amesema wanawake wako tayari na wamejipanga vizuri kuweze kutimiza malengo ya ushindi ya chama hicho.
Wakati huo huo Maalim Seif amezungumza na vijana wa barza wa Chama hicho katika maeneo ya Kidongo chekundu na Jang’ombe Urusi, na kuelezea dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kuwakomboa vijana.
Amesema amekuwa akijisikia vibaya wakati anapowaona vijana wakizurura mitaani bila ya kazi yoyote, jambo ambalo amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atalishughulikia tatizo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake.
Nao vijana hao wamemuhakikishia Katibu Mkuu huyo wa CUF kuwa wako makini na watalinda kura zao ili kuepuka ubadhirifu na wizi wa kura unaoweza kujitokeza.
Katika mkutano wa hadhara wa Chama hicho uliofanyika viwanja vya Kwabinti Hamrani Jang’ombe, Maalim Seif amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, Serikali yake itasimamia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuona kuwa mfumo huo unafika hadi ngazi za shehia.
Aidha amesema serikali yake itatenganisha majukumu ya chama na serikali, ili kuwaruhusu wataalamu na watendaji wa serikali kufanya kazi zao kwa uhuru bila ya kujihusisha na masuala ya kisiasa wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Maalim Seif alitumia mkutano huo kuwanadi wagombea Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa chama hicho kwa majimbo ya Jang’ombe na Mpendae.
from Blogger http://ift.tt/1J4QE91
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment