Historia inaibeba Yanga kuwa si timu inayoshindwa kirahisi kutwaa taji inapofikia hatua za mwisho za mbio za ubingwa.
Mbali na historia, mabingwa watetezi Yanga wana faida ya ratiba kuanzia raundi ya 23 baada ya kucheza pambano na watani wao wa jadi, Simba.
Yanga wamebakiza mechi mbili tu za mikoani na jambo zuri kwao ni kuwa mechi hizo zimepishana kwa mbali. Kama vile haitoshi, mechi yao ya Mtibwa Sugar inayotakiwa kuchezwa Morogoro inaweza pia kupigwa Dar kama uwanja wa Jamhuri utaendelea kufungiwa kutokana na ubovu wake.
Sio jambo la kushtua kusema kuwa Yanga wamebakiza mechi moja nje ya Dar wakati wapinzani wao, Simba wana mtihani wa mechi tatu za mikoani.
Wakati Yanga akiwa anateleza katika uwanja wa Taifa kwa kucheza mechi tano za nyumbani kati ya raundi ya 25 hadi 29, Simba atakuwa na kibarua cha kusaka pointi katika mechi tatu mfululizo Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar, Toto Africans na Mbao.
Kwa mahesabu haya, kuna dalili kubwa kwa mechi za raundi ya 25 hadi 28 kuamua bingwa kulingana na matokeo ya pambano la watani wa jadi yatakavyokuwa.
Licha ya takwimu kuonesha Simba ndio timu iliyochukua pointi nyingi ugenini, si rahisi kwao kuchukua pointi tisa katika mechi dhidi ya Toto inayopigania kutoshuka daraja, Kagera Sugar iliyoimarika chini ya Mecky Mexime na Mbao yenye matokeo ya kuridhisha ikiwa Mwanza.
Salama ya Simba ni kupata ushindi katika mechi ya watani wa jadi ili kutengeneza tofauti ya pointi tano na Yanga kwa kuwa ni rahisi kwao kudondosha pointi katika mechi tatu za Kanda ya Ziwa.
Endapo Simba wakifanikiwa kutengeneza tofauti ya pointi 5 ni wazi kuwa mbio za ubingwa zitaenda mpaka mechi ya mwisho ambayo inaweza kuwa faida kwa vijana wa Msimbazi kwani wanamalizia Dar wakati Yanga watakuwa Mwanza dhidi ya Mbao.
Hesabu nyingine ni kwa Simba ‘kuiombea Yanga dua mbaya’ ife mbele ya Azam katika mechi ya raundi ya 25.
Tisa kumi hesabu zote hizi zitategemeana na timu zote mbili kutoacha pointi kizembe katika mechi ambazo sare ni sawa na kufungwa.
Ikumbukwe msimu uliopita, wakati Yanga wakila viporo kwa ndimu, Simba ilitolewa katika mbio za ubingwa na timu ambazo kwa hesabu za haraka ilitarajiwa kubeba pointi tatu.
from Blogger http://ift.tt/2lO86PN
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment