Kufuatia malalamiko yaliyotolewa hivi karibuni na baadhi ya Watanzania wanaoishi na kufanya shughuli za kiuchumi katika mji wa Monte Puez ulioko Cabo Delgado nchini Msumbiji, kwamba wanafukuzwa, na kunyang’anywa hati za kusafiria pamoja na kuibiwa mali zao.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, leo imetolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo, ambapo imesema kuwa serikali ya Msumbiji imekiri kuwa na operesheni ya kuwakamata na kuwarudisha nyumba raia wa kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata sheria za uhamiaji za nchi hiyo. Ambapo hadi sasa watanzania zaidi ya 130 wamesharudishwa huku ikikadiriwa kuwa waliosalia wanafika 3000.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Suzan Kolimba, amesema waliofukuzwa waliingia nchini humo kinyume cha sheria, na kwamba wizara yake inaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania waliobaki na mali zao pamoja na wanaotakiwa kurudi .
“Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania nchini Msumbiji, na si watanzania pekee bali na raia wengine wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria,” amesema na kuongeza.
“Tumetuma balozi wetu na baadhi ya maofisa wa uhamiaji ili kujua ukweli kwa ajili ya kushughulikia suala hilo. Tunaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya nchi hiyo ili kuhakikisha usalama wa watanzania na mali zao.”
Katika hatua nyingine, Dkt Kolimba amesema wizara yake inaendelea kushughulikia watanzania nane waliokamatwa nchini Malawi na kwamba Waziri Augustin Mahiga alikwenda nchini humo kuonana na watanzania hao.
from Blogger http://ift.tt/2lQzk44
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment