NAIBU Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi, Mohammed Ahmada amekiri kuwepo kwa udhaifu wa ukaguzi
wa mizigo ya abiria katika bandari ya Malindi wakati wanapoingia nchini kutoka
sehemu nyingine na kuwepo tishio la kuingiza bidhaa na vitu mbalimbali haramu.
Ahmada alisema hayo wakati
alipozungumza na viongozi wa Shirika la Bandari na wakuu wa vyombo vya ulinzi
katika ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni
katika eneo la Bandari ya Malindi.
Alisema kuanzia sasa
utafanyika ukaguzi na kuhakikisha abiria wote wanaoingia nchini kutoka sehemu
mbalimbali ikiwemo Pemba au Tanzania Bara wanakaguliwa na kujua usalama wa
mizigo wanayoingiza nchini.
Alisema haiwezekani
kuwafanyia ukaguzi abiria katika kituo cha kwanza wanachotoka, lakini
ukashindwa kufanya ukaguzi katika kituo cha pili cha kuingia abiria ikiwa ndiyo
safari yake ya mwisho.
Alisema alizitaka mamlaka
pamoja na vyombo vya ulinzi kuimarisha ukaguzi wa aina hiyo katika bandari zote
kuu zikiwemo za Pemba na Mkokotoni, kwa upande wa Unguja.
Mkurugenzi wa Shirika la
Bandari la Zanzibar, Abdallah Juma alikiri kukabiliwa na uhaba wa mashine za
kisasa za kugundua vifaa mbalimbali vinavyoingizwa na abiria nchini.
Akizungumza na watendaji wa
shirika la bandari pamoja na vyombo vya ulinzi katika eneo hilo, naibu waziri
Masauni alitaka ulinzi uimarishwe katika vyombo vinavyotoa huduma za kubeba
mizigo ikiwemo majahazi.
Alisema wahalifu wamekuwa
wakibuni njia mbalimbali za kuingiza bidhaa hatari ikiwemo dawa za kulevya
ambapo hutumia majahazi yanayobeba mizigo mbalimbali kuingiza dawa hizo.
0 maoni:
Post a Comment