MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amelaani na kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji, vinavyoendelea katika jamii na kutaka wananchi kushirikiana katika kukabiliana na vitendo hivyo nchini.
Mama Samia alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Alisema vitendo hivyo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji, vinamchukiza na kusisitiza kuwa ni wakati sasa wananchi na wadau wote bila kujadili dini, kabila wala rangi, kupambana ipasavyo na vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, alisema anafurahishwa na hatua na jitihada zinazochukuliwa na wanawake nchini katika kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Katika hatua nyingine, wanafunzi 78 wa shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Dodoma, wamegundulika kuwa ni wajawazito.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo katika wilaya ya Dodoma Mjini, wanawake walitembelea na kwenda kutoa msaada kwenye Kituo cha Walemavu wa Akili cha Miyuji.
Mkoani Kilimanjaro, wanawake wametakiwa kutumia fursa zilizopo mkoani humo, kwa kuhamasisha jamii kupanda Mlima Kilimanjaro na kuutangaza mti mrefu kuliko yote Afrika, uliogundulika katika Hifadhi ya Mlima huo (Kinapa).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), Joyce Msiru, alisema hayo wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu Siku ya Wanawake Duniani inayokwenda na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya Viwanda, Wanawake ndio Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi”.
Msiru alisema wanawake wana nguvu, hivyo wasikae na kujiona wanyonge, badala yake wajihusisha kwenye shughuli za kuleta maendeleo ya nchi na kufanyakazi kwa bidii.
Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, wanawake wametakiwa kutumia fursa walizonazo, kuondokana na woga katika kujitosa kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Rai hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani na Kaimu Mkuu wa Mkoa, Felix Lyaviva kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, wakati alipozungumza na maelfu ya wanawake wa jiji hilo waliojitokeza kuadhimisha siku hiyo.
Alisema hakuna mtu yeyote duniani, aliyeanza biashara na kwa muda mfupi akawa tajiri kwani wengi wao wameanzia chini na baadaye kutokana na juhudi zao wamejikuta wakiwa na mafanikio makubwa.
Nao wanawake mkoani Mbeya wamehimizwa kutumia busara, wanapodai haki zao za msingi kwa waume zao, kwa kuwa kutumia jeuri na kiburi, kunaweza kuwasababishia kukosa haki hizo na kuleta mvurugano katika familia zao.
Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa alisisitiza hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika kimkoa jijini Mbeya na kuhudhuriwa na wanawake kutoka kada mbalimbali.
Dk Mwanjelwa alisema kumekuwepo na baadhi ya wanawake, ambao kwa kuwa tu wanadai haki za msingi, basi wamekuwa wakitumia njia zisizostahili ikiwemo kiburi na dharau kwa waume zao.
Katika hatua nyingine, Halmashauri za miji/wilaya na majiji nchini, zimeagizwa kutenga maeneo maarufu ya biashara kwa wanawake ili kuwawezesha kuyatumia kwenye shughuli za kibiashara na uwekezaji wa ndani ili kuinua vipato vyao.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Dk Anjeline Mabula wakati alipokuwa akihutubia mamia ya wanawake wa mkoa wa Mwanza kwenye kilele cha Siku ya Wanawake duniani, yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha katika Manispaa ya Ilemela.
Alisema baadhi ya wanawake wengi, hawana uwezo wa kumiliki ardhi na kuwa inakuwa ni vigumu kwao kukopesheka kwenye taasisi za fedha, zikiwemo benki. Alitaka halmashauri hizo, kutenga maeneo kwa ajili ya ustawi wa shughuli zao za kiuchumi.
0 maoni:
Post a Comment