Baada ya maandamano ya wasanii wa filamu nchini yaliyofanyika Jumatano hii katika mtaa wa Aggrey Kariakoo, msanii wa tasnia hiyo Steve Mengele Nyerere amefunguka kuhusu tukio hilo.
Akiongea na waandishi wa habari, Steve ameeleza kuwa sababu ya yeye kutokuungana na wasanii wenzake kuandamana ni kwa kuwa jambo hilo halioni kama lina tija kwake.
“Binafsi ninalipinga hili, wasanii tunataka kutumika ndivyo sivyo. Mimi siwezi tu kuambiwa kuwa kuna maandamano nikaenda.
“Tunavyosema filamu za nje zinazuia soko la ndani ni uongo, hizi filamu za nje tangu tunazaliwa zilikuwepo, tumewakuta akina Arnold Schwartzneger na Rambo, filamu zao zilikuwa zinauzwa Kariakoo. Tulizichukua majority tukatengeneza filamu zetu. Tuliwakuta wanigeria tukashindana nao tukaweza, hata filamu za Kihindi tuliweza kushindana nazo.
“Hatujawahi kumzuia Yemi Alade afanye muziki hapa nchini ijapokuwa tuna wanamuziki wetu akina Diamond na Ali Kiba.
“Ninachoweza kusema ni kwamba turudi tuangalie ni wapi tumeharibu, tuache kuingiza visingizio ambavyo havina mantiki. Wafanyabiashara Kariakoo wanauza filamu zinazouza na siyo uzalendo.
“Watanzania tumezoea kukaa mezzani na siyo maandamano. Utazuia Dar, je vipi kuhusu Arusha, Dodoma, Mwanza nk… hili janga sio la Dar es Salaam pekee ni la Tanzania nzima.
“Mpaka sasa msambazaji ni mmoja, aliyelemewa mzigo. Serikali iruhusu wasamazaji wengine wafanye kwenye biashara hii.”
“Tumeshindwa kutengeneza ladha ya Watanzania, tusiwaadhibu wafanyabiashara, tujiadhibu sisi wenyewe kwa kutengeneza filamu zisizouza.” Alisema Steve Nyerere.
0 maoni:
Post a Comment