Aveva alidai Simba haikutendewa haki kutokana na kanuni za ligi kuu kuonesha walipaswa kuachiwa pointi 3 na mabao matatu kama ilivyoamriwa na kamati ya saa 72, lakini cha kushangaza kamati ya Sheria, Katiba na hadhi za wachezaji ya TFF ilizirejesha alama na mabao hayo Kagera Sugar.
Mratibu wa kikosi cha Kagera Sugar, Mohamed Hussein amesema suala la Simba kutaka kwenda CAS ni haki yao na itakua vyema kutokana na utata uliopo, ambao umekua ukiwachanganya wadau wa soka nchini.
Mohamed amesema wanaamini haki inatafutwa kwa kufuata taratibu na sheria, na waliposikia kauli ya Aveva aliyoitoa juzi walifarijika kutokana na jambo hilo litaendelea kutolewa ufafanuzi zaidi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za ligi kuu.
Hata hivyo Mohamed Hussein, amehoji kwa nini Simba wamekua na uchungu na pointi 3 ilihali hawakujitahidi uwanjani siku ya mchezo na badala yake walikubali kufungwa mabao mawili kwa moja.
“Simba wakubali kwanza tuliwafunga uwanjani, na hata kama wanakwenda CAS watambue tuliwafunga, jambo ambalo lilikua sahihi kwetu kupata point tatu, na ndio maana tulirejeshewa pointi zetu na kamati ya Sheria ya TFF,“Alisema Mohamed kwenye mahojiano yake na Times FM na kusisitiza kuwa wanawaunga mkono kusonga mbele
“Tunawatakia kila la kheri huko waendapo na tunaamini haki itaendelea kuonekana imetendeka, kutokana na wenzetu kupiga hatua zaidi katika masuala ya maendeleo ya soka, hasa linapokuja suala lenye utata la mchezaji kuonyeshwa kadi kama hili.” Alisema Mohamed Hussein.
Simba SC wanasubiri barua ya hukumu iliyotangazwa na kamati ya Sheria, Katiba na hadhi za wachezaji kutoka TFF, ili waanze mchakato wa kupeleka malalamiko yao CAS ambapo wanaamini watafanikisha mpango wa kuzipata pointI na mabao matatu dhidi ya Kagera Sugar.
By Godfrey Mgallah
0 maoni:
Post a Comment