Marekani yataka Iran ishiriki vita dhidi ya Dola la Kiislamu

Marekani inakiri kuwa hata adui mkubwa, Iran, ana wajibu mkubwa kwenye kulishinda kundi linalojiita "Dola la Kiislamu" ambalo limeshachukuwa eneo kubwa la mataifa ya Syria na Iraq.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akizungumza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, akizungumza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza kwenye kikao cha mawaziri wa nje wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Kerry alisema katika juhudi za pamoja za kimataifa dhidi ya kitisho cha kundi hilo, "takribani kila nchi ina jukumu la kutekeleza, ikiwemo Iran."
Wiki hii, Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alisema alikuwa amelikataa ombi la Marekani la kushirikiana nayo kwenye uwanja wa mapambano. Ingawa maafisa wa Marekani hawajathibitisha wala kukanusha kutuma ombi hilo, lakini kimsingi wamekuwa hawaichukulii Iran kuwa sehemu ya muungano wanaouunda kupambana na Dola la Kiislamu.
Wiki iliyopita, mwanadiplomasia mmoja wa ngazi za juu wa Marekani alisema lisingelikuwa jambo muafaka kuialika Iran kwenye mikutano inayojaribu kujenga muungano huo wa kimataifa kutokana na "kujihusisha kwa serikali ya Iran nchini Syria na kwengineko."
Kwa upande mwengine, Iran inaziunga mkono serikali za Iraq na Syria katika vita vyao dhidi ya kundi hilo la Dola la Kiislamu.
Maelfu ya Wakurdi wa Syria waingia Uturuki
Basi lililobeba mateka 49 wa Kituruki waliochiwa huru na Dola la Kiislamu katika uwanja wa ndege wa Sanliurfa, Uturuki. Basi lililobeba mateka 49 wa Kituruki waliochiwa huru na Dola la Kiislamu katika uwanja wa ndege wa Sanliurfa, Uturuki.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Numan Kurtulmus, alisema siku ya Jumamosi (Septemba 20) kwamba maelfu ya Wakurdi wa Syria walivuuka mpaka na kuingia nchini Uturuki siku ya Ijumaa wakiwakimbia wapiganaji wa Dola la Kiislamu ambao wamesonga mbele na kuteka vijiji kadhaa karibu na mpaka.
"Kiasi cha Wakurdi 45,000 wa Syria wamevuuka mpaka kupitia milango minane kwenye masafa ya kilomita 30 kutoka Akcakale hadi Mursitpinar tangu tuufunguwe mpaka jana," waziri huyo aliiambia idhaa ya Kituruki ya televisheni ya CNN.
Uturuki ililazimika kufungua sehemu ndogo ya mpaka huo hapo Ijumaa baada ya raia hao wa Kikurdi kukimbia makaazi yao, wakihofia mashambulizi kwenye mji wa Ayn al-Arab ulio mpakani mwa Syria.
Kusonga mbele kwa wapiganaji wa Dola la Kiislamu kaskazini mwa Syria kumesababisha wito wa msaada kutoka kwa Wakurdi kwenye eneo hilo, wanaohofia mauaji ya maangamizi kwenye mji huyo wa Ayn al-Arab, unaoitwa Kobani kwa Kikurdi. Mkuu wa wapiganaji wa Kikurdi wanaoulinda mji huo, Esmat al-Sheikh, alisema mapigano yalikuwa yakiendelea kaskazini na mashariki mwa mji huo siku ya Jumamosi.
"Wapiganaji wa Dola la Kiislamu wakitumia maroketi, mizinga, vifaru na magari yenye silaha nzito wamesonga mbele kuelekea Kobani usiku wa jana na sasa wako umbali wa kilomita 15 kutoka hapa mjini," aliliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.
Shirika la Haki za Binaadamu la Syria linalofuatilia hali ya mambo huko, linasema kiasi cha wapiganaji 18 wa Dola la Kiislamu waliuawa kwenye mapigano na Wakurdi wa Syria hapo usiku ingawa kundi hilo limechukuwa udhibiti wa vijiji zaidi vinaouzunguka mji huo muhimu kwenye mpaka wa Uturuki na Syria.
Mateka wa Uturuki waachiwa huru
Wakimbiri wa jamii ya Wakurdi wa Syria wakivuuka mpaka kuingia Uturuki. Wakimbiri wa jamii ya Wakurdi wa Syria wakivuuka mpaka kuingia Uturuki.
Katika hatua nyengine, Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu amesema raia 49 wa nchi yake waliokuwa wakizuiliwa na wapiganaji wa Dola la Kiislamu nchini Iraq wameachiwa huru leo na wamerejea nyumbani salama. Davutoglu alikutana na mateka hao katika jimbo la Sanliurfa mji ulioko mpakani na Syria, mara tu baada ya kuachiwa huru.
Waturuki hao walitekwa nyara kutoka ubalozi mdogo wa Uturuki mjini Mosul nchini Iraq tarehe 11 Juni 2014, wakati wapiganaji hao wenye itikadi kali walipoudhibiti mji huo. Kuachiwa huru kwa raia hao wa Uturuki kunakinzana na vitendo vya kukatwa vichwa kwa raia wawili wa Marekani na mmoja wa Uingereza na wapiganaji wa Dola la Kiislamu.
Haijabainika wazi ni kipi serikali ya Uturuki imefanya kuhakikisha raia wake wameachiwa huru. Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuachiwa huru kwa raia wake ni kutokana na operesheni iliyokwenda vyema.
Naye kiongozi wa jimbo la Kurdistan nchini Iraq, Masoud Barzani, hapo Ijumaa alitoa wito kwa uingiliaji wa kimataifa kuulinda mji wa Kobani dhini ya kusonga mbele wa Dola la Kiislamu, akisema waasi hao lazima "wapigwe popote walipo."
Kampeni ya kimataifa dhidi ya Dola la Kiislamu inayoongozwa na Marekani dhidi ya Dola la Kiislamu hadi sasa haijaweka bayana namna itakavyokabiliana na waasi hao ndani ya ardhi ya Syria.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
 Mhariri: Caro Robi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment