WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea
wanaoidai fidia ya sh. bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na
kuwa eneo la kiuchumi mkoani Ruvuma (Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa
viwanda.
Ametoa
ahadi hiyo leo (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na
wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Manispaa hiyo.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano inatambua kilio chao ambacho alisema ni cha
muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa mbunge wao
wa zamani, Bw. Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu.
“Alipotoka
kutibiwa India alikuaja ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo
mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie
ufumbuzi. La kwanza lililkuwa ni hili la fidia kwa wakazi wa
Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi wa kituo cha mabasi cha
mabasi cha mjini Songea,” alisema.
“Leo
nimefanya ziara maalum kwa ajili yenu kwa sababu serikali ya awamu ya
tano iko kwa ajili yenu na hasa wananchi wanyonge. Na tatizo hili
inalijua. Kabla sijafika hapa, nilipita kwenye eneo husika na afisa
mipango miji akanionyesha ramani ya eneo lenu hili,” alisema.
Waziri
Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari
wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu.
“Kutakuwa
na kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe
na mbolea. Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu
kitakuwa ni cha kukamua mafuta ya mbegumbegu,” alisema na kuongeza
kwamba reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbaba Bay inatarajiwa kupita kwenye
eneo hilo.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa amlipo yao, Waziri Mkuu alisema kwamba
katia ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu, na
kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na
mnunuzi wa eneo husika.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa ulipaji kwa
sababu walifuata orodha ya majina (kialfabeti) badala ya kutoa malipo
kwa wakazi wa eneo husika. “Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza ujenzi,
lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo
hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe. Serikali itawafuatilia
hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia
waweze kulipwa,” alisema.
Jumla
ya watu 2,179 walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika
kuwa ni sh. 3,254,737,622. Kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa
wakazi 1,179 sh. 1,920,242,121 ambapo kati ya hizo, sh. 1,210,078,261
zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za wananchi na sh. 710,163,860
zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.
Eneo
hilo lenye ukubwa wa hekta 2,033 (sawa na ekari 5,000) lilitwaliwa na
Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa kushirikiana na uongozi
wa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea tangu mwaka 2007. Eneo hilo
linajumuisha mitaa ya Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na Luhira.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Afisa Ardhi wa Manispaa ya Songea, Bw.
Kundaeli Fanuel Ndemfoo afuatilie suala la Bibi Monica Joseph Miti na
wanae ambao walidhulumiwa nyumba ya urithi na aliyekuwa mwanasheria wa
manispaa hiyo.
Ametoa
agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya
Mwengemshindo baada ya kupokea bango lililoandikwa na Bibi Miti kuomba
arejeshewe umiliki wa nyumba ya marehemu muwewe.
Alipopewa
nafasi ya kueleza tatizo lake, Bibi Miti ambaye alimtaja mwanasheria
huyo kwa jina moja la Bw. Mwakasungura, alidai kuwa mwanasheria huyo
alighushi hati ya nyumba, na kuwatoa ndani ya nyumba yeye na watoto wa
marehemu.
Alipoulizwa
na Waziri Mkuu aeleze alipo huyo mwanasheria wa manispaa, Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Bibi Tina Sekambo alijibu kwamba alishahamishiwa wilaya
ya Ukerewe.
Waziri
Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Ardhi wa
Manispaa wafuatilie suala hilo na wampe majibu mapema iwezekanavyo. Pia
amemuomba Bibi Miti na wanawe wafike kuonana naye Januari 3, mwakani
atakapokuwa Songea kwa mapumziko mafupi ya mwisho wa mwaka.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Ruvuma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 maoni:
Post a Comment